Rushwa: Kikwete,alinunuliwa nguo za suti huko London na Ali Albwardy wa Falme za Kiarabu.

Jakaya Kikwete

Jakaya Kikwete

Kikwete, Wikileaks na suti za Mwarabu!

Source: http://www.raiamwema.co.tz/kikwete-wikileaks-na-suti-za-mwarabu

KAMA kuna wakati nimefurahia maelezo ya Ikulu, ni yale ya kina yaliyotolewa juzi (Jumatatu) ya kukanusha habari zilizoripotiwa na mtandao wa Wikileaks zilizodai kuwa Rais Kikwete, alipokuwa waziri na mgombea urais wa CCM, alinunuliwa nguo za suti huko London na mfanyabiashara  Ali Albwardy wa Falme za Kiarabu.

Maelezo hayo, yenye lugha kali, yalijaribu kuwashawishi Watanzania – lakini naamini yaliandikwa kwa ajili ya watu wa nje zaidi – kuwa taarifa za Wikileak hazikuwa na ukweli wowote.

Taarifa za wikileak zilitegemea nyaraka za siri ambazo Ubalozi wa Marekani nchini ulikuwa unakusanya na kupelekeana na wanadiplomasia wake. Nyaraka hizo za mawasiliano ya kibalozi zinajulikana kama diplomatic cables, kimsingi, ni maelezo ya wazi kabisa na yasiyo na kujificha juu ya maoni ya wanadiplomasia katika balozi kwenda kwenye wizara za mambo ya nchi za nje za nchi zao. Kila taifa lina maelezo yake ya ndani kwa ndani kati ya maafisa wa ubalozi na serikali zao.

Ni nyaraka hizi ndizo zinazofungua mawazo ya balozi mbalimbali kuhusu viongozi na maisha kwenye nchi ziliko balozi hizo. Kutokana na uwazi wake, nyaraka hizo za kidiplomasia kwa kawaida kabisa huwa ni za siri sana.

Kufunuliwa kwa nyaraka hizo kulisababisha maneno makali kutoka nchi mbalimbali; kwani baadhi ya mambo ambayo maafisa wa serikali hiyo walidhania ni siri yaliwekwa hadharani na wakati mwingine bila kuficha vyanzo vya habari.

Kwa mfano, hapa Tanzania kuna mambo yaliyodaiwa na Dk. Hosea wa TAKUKURU kuhusu ugumu wa yeye kupambana na rushwa kubwa. Sehemu nyingine duniani taarifa hizo zilisababisha watu kujiuzulu; kwani mambo yaliyoripotiwa yalikuwa yanatishia kabisa kuaminiwa kwao na serikali zao.

Mapema mwaka huu, Balozi wa Marekani huko Mexico, Bw. Carlos Pascual, alijiuzulu wadhifa wake baada ya Wikileaks kuonesha kuwa alitoa maoni makali juu ya vyombo vya usalama vya Mexico vinavyogombana vyenyewe kwa vyenyewe na hivyo kufanya mapambano dhidi ya vikundi vya wauza madawa ya kulevya kuwa magumu.

Huko Honduras Balozi wa Marekani alitakiwa kuondoka kutokana na yale ambayo alinukuliwa kusema kwenye nyaraka hizo za kidiplomasia.

Kwa ufupi, mtu anayejaribu kupuuzia yale yaliyomo humo anataka watu wachukulie kirahisi rahisi yanayosemwa au kutokujali. Ikumbukwe pia kwamba taarifa hizo za kidiplomasia hazikuwa kwa ajili ya hadharani hivyo, kwa hiyo hakukuwa na sababu yoyote ya wasemaji wanaonukuliwa kusema vitu ambavyo wanajua vingewaletea matatizo.

Na ni wazi  kwamba watu hao wakiulizwa, ni vigumu kukubali kuwa walisema hivyo; kwani mazungumzo yao na viongozi wa Marekani yalikuwa yawe ya siri.

Ni kutokana na hilo basi, yanayosemwa na Wikileaks kuhusu Kikwete, japo Ikulu wanataka yapuuziwe, yanahitaji maelezo ya kushawishi akili zaidi kuliko kutuambia tu ni uongo wa kutupwa.

Maelezo yaliyotolewa na Ikulu yetu yamekanusha mambo mawili makubwa; Kwanza, kwamba Rais Kikwete alikubali kufadhiliwa safari na nguo na Bw. Ali Albwardy na pili kwamba kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2005, chama chake kilipokea msaada wa karibu Shilingi bilioni moja kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Kwenye suti, balozi wa Marekani wa wakati huo, Bw. Michael Retzer, anasema wazi kuwa: “Rais Kikwete alipokea zawadi (rushwa) kutoka kwa mmiliki wa mahoteli ya Kempinski” na kuwa katika mazungumzo yake na afisa uhusiano wa hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Bi. Lisa Pile, alimwambia kuwa “hivi karibuni Bw. Ali Albwardy alimgharimia safari Kikwete huko London kufanya manunuzi. Katika safari hiyo Ali Albwardy alimnunulia Kikwete suti tano za Saville Row. Hivi karibuni ametoa mchango wa dola milioni moja kwa CCM”.

Haya si madai ya kupuuzia tu kirahisi. Binafsi, ningependa kuingia kwa undani kwa kuangalia madai ya nyaraka hizo na majibu ya serikali yaliyotolewa siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, sitafanya hivyo kwa sasa; kwani majibu ya serikali yamenifanya niulize swali ambalo bila ya shaka watu wengine wangependa kupata majibu yake vile vile.

Katika majibu yaliyotolewa na Ikulu ambayo, kama nilivyosema, yalijaa maneno makali ya kuvuta  hisia – siyo hoja nzito – tunakutana na mambo ambayo yameacha maswali mengine zaidi.

Kuhusu mchango wa Sh. bilioni moja

Maelezo ya nyaraka za Wikileak yanaonesha kuwa anayedaiwa kutoa fedha hizo ni Bw. Ali Albwardy kwenda kwa CCM. Hapa, naomba niweke maneno yenyewe ya Kiingereza ili nisije kudaiwa kuwa labda ninaikoroga “lugha ya Malkia”. Balozi Retzer ananukuliwa kusema “I learned later in the evening from hotel publicity director Lisa Pile (protect) that the hotel owner, UAE citizen Ali Albwardy, had recently flown Kikwete to London for a subsidized shopping expedition.Among other things, on that trip Ali Albwardy bought Kikwete five Saville Row suits. He had also recently made a $1 million cash contribution to the CCM (which is a legal contribution under current Tanzanian law)”

Sasa ni wazi kuwa inaposemwa kuwa “he had also recently” haimaanishi kampuni ya hoteli Kempinski; bali mmiliki wake kama mtu binafsi. Hii ni kweli pia kwa sababu sentensi inayofuatia inatokana na hiyo ya nyuma ambayo inamzungumzia Bw. Ali mwenyewe na siyo hoteli yake.

Jibu la serikali linasema hivi katika mlolongo wa makanusho yake kuwa: “The president was not responsible for raising nor receiving campaign funds for CCM party during 2005 General Elections. He was simply the flag bearer of the party. However, he is privy to information that Kempinski Kilimanjaro Hotel was never asked no contributed a single cent towards CCM campaign. Therefore the allegation that Kempinski Kilimanjaro Hotel contributed one million (USD1,000,000) toward CCM campain are baseless and unfounded”.

Sasa mtu yeyote mwenye ujuzi mdogo tu wa lugha ya Kiingereza anaweza kuona kabisa kuwa Ikulu haikujibu hoja ya Bw. Ali Albwardy kuichangia CCM shilingi bilioni moja hizo.

Serikali imekanusha kuwa hoteli haikuchangia – kitu ambacho nyaraka za kidiplomasia hazidai! Je, Ikulu  wamefanya hivyo kwa bahati mbaya au ni kujaribu kupotosha kwa makusudi? Je yawezekana ni kweli kuwa Bw. Albwardy aliichangia CCM yeye binafsi? Kwa Ikulu kuchagua kujibu swali lisilo swali, wametoa jibu la swali wasilotaka kuulizwa.

Labda hapa tuulize kitu kingine ambacho wengine tunakikumbuka. Wakati wa kampeni ya mwaka 2005 kulikuwa na taarifa kuwa kampeni ya Kikwete ilipokea kiasi cha dola milioni 2, na ni kiasi ambacho kilikwenda kwa Kikwete.

Lakini Kikwete (wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje) alikanusha vikali taarifa hizo na kutishia kwenda mahakamani kulishitaki  jarida la Africa Confidential lililoandika habari hizo. Gazeti  lilimuambia aende; kwani lina ushahidi wa kutosha. Kitu ambacho kinaacha swali ni kuwa taarifa za wakati huo zinaonesha fedha hizo zilikuwa kutoka Oman na baadaye Mtikila aliwahi kudai dola milioni 2 nyingine zilikuwa kutoka Iran.

Sasa, hizi taarifa za sasa za kupewa milioni moja toka kwa mtu binafsi zaweza kuwa na ukweli kiasi gani? Kwa nini Rais Kikwete anahusishwa na taarifa hizi za kupokea fedha nyingi kiasi hiki kutoka nje ya nchi? Kwa nini iwe yeye na si kiongozi mwingine?

Suala la kununuliwa suti

Lakini hayo maswali bado hayajanisumbua sana kama majibu ya Ikulu  kuhusu gharama za nguo za Kikwete. Taarifa ya Ikulu kwenye kipengele cha 4 tunaambiwa kuwa Rais Kikwete hajawahi kukutana na Albwardy huko London kwa manunuzi yoyote na kuwa “In any case, as Foreign Minister he is (was) given adequate clothing allowance. And now as (the) President his clothing is the responsibility of the state” Tafsiri isiyo rasmi ya maneno hayo ni  kuwa alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje alipokea posho ya mavazi na kuwa sasa kama Rais mavazi yake yanagharimiwa na serikali.

Hapa ndipo nimejikuta nikijuliza swali ambalo pia nilijiuliza wakati tulipoambiwa kwamba wabunge wanaposafiri nje ya nchi wanapewa posho ya mavazi! Nimebakia kujiuliza: Hivi hawa wenzetu mishahara yao wanafanyia nini?

Yaani; kama kula wanalishwa na serikali, wanasafirishwa na serikali, wanalindwa na serikali, hadi wanavalishwa na serikali –  wao mishahara yao inafanyiwa nini?

Hivi ni Mtanzania gani ambaye anafanya kazi ambaye asingependa kuona anafanyiwa kila kitu; huku mshahara wake anadunduliza tu benki? Kikwete kama Rais tayari anasafiri sana, na kwa miaka mitano iliyopita amesafiri sana na kama toka akiwa Waziri wa Mambo ya Nje amekuwa akipokea posho ya mavazi, hivi hadi hivi sasa tunajua Watanzania wametumia kiasi gani kumvisha Rais wao?

Jibu ambalo tunaweza kupewa ni kuwa “hatutaki Rais wetu aonekane amevaa matambala au nguo zisizoendana na hadhi yake” . Hilo sawa; lakini kwa nini asinunue kwa mshahara wake?

Hili linanileta kwenye swali ambalo Ikulu ninawapa walijibu sasa kwa uwazi tu kama walivyofanya kwenye hili: Rais Kikwete analipwa mshahara wa kiasi gani kwa mwezi na posho gani ambazo anazipata kwa mwezi? Tayari tunajua anapata posho ya mavazi, je anapokea pia posho ya vikao vya baraza la mawaziri?

Vipi kuhusu posho za kusafiri mikoani au kuzungumza kwenye taasisi binafsi? Je anapokea posho kiasi gani kwa siku anapokuwa nje ya nchi?

Kama Watanzania ndio wanagharimia hadi mashati, suruali na viatu vya Kikwete, wanayo haki ya kujua wanalipia kiasi gani.

Lakini zaidi ni kuwa kama Rais Kikwete hatumii mshahara wake kujihudumia yeye mwenyewe wakati umefika kwa Rais Kikwete kuonesha mfano kwa kurudisha kiasi chote ambacho Watanzania wamemlipia kumvalisha katika nguo zake anazopendeza.

Ninaposema “chote” ninamaana ipigwe hesabu ya kiasi chote alichopokea kwa posho ya mavazi na akirudishe kwa Watanzania. Atumie mshahara wake kujinunulia nguo!

Hatujatengeneza ufalme hapa Tanzania! Hata wafalme kama kule Uingereza wanajigharimia vitu vyao vingi wao wenyewe siyo kila kitu kinagharimiwa na Waingereza. Au watu wamesahau jinsi Prince William na mke wake Katie walivyojigharimia wenyewe kupanda ndege hivi majuzi tu tena daraja la tatu la wenzangu na miye?

Pendekezo jingine ni kuwa Ikulu itoe tamko jingine na kukanusha madai kuwa Rais Kikwete anapokea mshahara mnono na posho kubwa kubwa ambazo hazitumii kwa lolote lile kiasi ambacho kinadaiwa kuwa kinakaribia shilingi milioni 20 kwa mwezi!

Kama ni kweli, na hatumii fedha hizi kununulia nguo zake mwenyewe, viatu, saa na mikanda au hata kununulia perfume na tai, kuna jina moja tulikuwa tunalisema enzi zile za Mwalimu.

Jina ambalo leo hii halitajwi tena wala kuzungumzwa hadharani; jina ambalo wakati ule ukilitaja kumuelezea mtu mwingine ilikuwa inatisha na kumfanya mtu huyo aonekane ni tatizo kwa jamii. Jina la wale ambao mirija yao ilikatwa na Azimio la Arusha.

Kama hulijua jina hilo muulize mzee aliyeko karibu ukimpa dalili hizi nilizozitaja humu. Utashangaa wazee wote watajua jina la kumuita mtu huyo!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s